Friday, September 16, 2011

Kundi la Muziki wa taarabu la T-Moto limesogeza mbele uzinduzi wa albamu yake ili kuomboleza msiba wa meli ya Mv Spice Islander's




Kundi jipya la Taarab la Tanzania Modern Taarab (T-Moto) limesogeza mbele uzinduzi wake uliokuwa ufanyike Septemba 30 mwaka huu hadi Oktoba 28.

Kundi hilo lililoondoka jijini na kuweka kambi ya maandalizi katika Visiwa vya Zanzibar hivi karibuni limeamua kusimamisha mazoezi yake kwa muda wa wiki moja na nusu kufuatia msiba mkubwa ulioikumba nchi kutokana na ajali ya meli ya Mv SPICE ISLANDER'S iliyozama eneo la Nungwi hivi karibuni na kusababisha vifo vya watu wengi na majeruhi ikiwa ni idadi ambayo haijawahi kutokea ndani ya Visiwa hivyo.

Mkurugenzi wa kundi hilo, AMIN SALMIN ambaye ni mtoto wa Rais Mstaafu wa Zanzibar, SALMIN AMOUR ‘Komandoo’, amesema kutokana na kundi hilo kutambua ukubwa wa msiba huo ulio na idadi kubwa ya vifo vya watu kulinganisha na idadi ndogo ya watu waishio visiwani humo, wameamua kusitisha kambi ya mazoezi yao ikiwa ni sehemu ya kundi hilo kuwa katika maombolezo.

Amesema kuwa wasanii wa kundi hilo wataendelea kubaki kambini bila kuendelea na mazoezi hayo ya maandalizi ya uzinduzi wao, hadi baada ya wiki moja na nusu kuanzia siku ya kwanza kati ya tatu za maombolezo zilizotangazwa na Serikali ya Zanzibar.

Kundi hilo linatarajia kuwasili jijini wiki ijayo kwa ajili ya kuingia studio kurekodi nyimbo zake mbili zilizokwisha kamilika na kurejea tena Zanzibar kuendelea na kambi hiyo

Thursday, September 15, 2011

Bodi ya wakurugenzi wa kampuni ya Etisalat yakutana na Dakta Shein Ikulu ya Zanzibar



Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dakta ALI MOHAMMED SHEIN akizungumza na Uongozi wa Bodi ya wakurugenzi ya Kampuni ya Etisalat, walipofika Ikulu mjini zanzibar kumpa pole Rais, kutokana na ajali ya kuzama kwa Meli ya Mv SPICE ISLANDERS, iliyokuwa ikielekea kisiwani Pemba.

Rais wa Visiwa vya Comoro Dakta IKILILOU DHOININE awasili nchini


Rais wa Visiwa vya Comoro Dakta IKHILILOU DHOININE amewasili nchini leo mchana akiwa ameambatana na ujumbe wake na kupokewa na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dakta JAKAYA KIKWETE.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na maofisa wa Comoro zimeeleza kwamba lengo la ziara ya Dakta DHOININE ni kutoa pole kwa rais KIKWETE kutokana na vifo vya wananchi vilivyotokana na ajali ya meli ya Mv SPICE ISLANDER iliyokuwa ikitokea Unguja kuelekea Pemba.

Wednesday, September 14, 2011

Ujumbe wa Chama cha Mapinduzi CCM watoa Pole kwa rais wa Zanzibar Dakta Ali Mohammed Shein


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ,Dakta ALI MOHAMMED SHEIN akisalimiana na Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara PIUS MSEKWA akiongoza ujumbe wa CCM uliofika Ikulu Mjini Zanzibar,kumpa pole kutokana na Msiba kwa wananchi,waliofariki kwa ajali ya Meli ya Mv SPICE ISLANDER ambayo ilizama Ijumaa ya wiki iliyopita huko Bahari ya Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja ilipokuwa ikielekea Pemba.

Makamu wa rais Dakta Mohammed Gharib Bilal ahudhuria Maonesho ya Miaka 35 ya Utendaji kazi wa reli ya Tazara


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dakta MOHAMMED GHARIB BILAL akisoma hotuba yake wakati wa maadhimisho ya Kumbukumbu ya miaka 35 ya reli ya TAZARA kuelekea maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania.




Balozi wa Zambia hapa nchini MAVIS LENGALENGA (kushoto) akicheza ngoma ya asili iliyokuwa ikitolewa na kikundi cha Sanaa cha Makanjani kutoka Zambia, wakati wa maadhimisho ya Kumbukumbu ya miaka 35 ya reli ya Tazara kuelekea maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania, Maonyesho hayo yamefanyika katika Viwanja vya Tazara jijini Dar es Salaam.

Sunday, September 11, 2011

Idadi ya waliofariki katika ajali Mv Spice Islander yafikia 240,huku jitihada ya uokoji wa manusura na miili zikiendelea eneo la Nungwi visiwani Zanzibar.




Baadhi ya wanajeshi wa kikosi cha kutuliza ghasia FFU pamoja na wanaharakati wengine wa uokozi wakibeba majeruhi aliyenusurika na kifo katika ajali ya kuzama kwa Meli ya Mv SPICE ISLANDER,katika ufukwe wa bahari ya Nungwi Mkoa wa kaskazini Unguja.

Makamu wa rais Dakta Mohammed Gharib Bilal atembelea Majeruhi wa Ajali ya Mv Spice Islander


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dakta MOHAMMED GHARIB BILAL Mama ZAKHIA BILAL na Mama ASHA BILAL, wakiwa katika viwanja vya Hospitali ya Mnazi Mmoja, wakati alipofika kuwajulia hali majeruhi wa ajali ya Meli ya Mv SPICE ISLANDER iliyotokea eneo la Nungwi Pemba.



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dakta MOHAMMED GHARIB BILAL akimjulia hali mmoja kati ya majeruhi wa ajali ya Meli, MUSSA HEMED, mkazi wa Wete Pemba, aliyelazwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja mjini Zanzibar.