Hali ilivyokuwa leo Asubuhi katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar
Kiongozi wa Jumuiya ya kikundi cha uamsho, Sheikh FARID HADI AHMED
|
Maelfu wa Wazanzibari wakiongozwa na Taasisi za Kiislamu na Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar JUMIKI, wakifanya matembezi ya amani katika barabara za Zanzibar na kupeleka ujumbe wao kwa viongozi wa Serikali ya Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Umoja wa Mataifa wakitaka Zanzibar huru, ambapo baadhi ya watembeaji hao wakiongozwa na Kiongozi wa Jumuiya hiyo, Sheikh FARID HADI AHMED na viongozi wengine.
Na ; Mwandishi wetu
Waandamanaji hao wakiongozwa na Sheikh Farid Hadi Ahmed walitembea kutoka viwanja vya Lumumba na kupitia barabara ya Kinazini, Mpigaduri, Michenzani Maskani ya CCM Kisonge, kwa Biziredi na kurudi tena viwanja vya Lumumba.
Maandamano walioyaita matembezi ya amani yalifanyika na kuhudhuriwa na maelfu ya wazanzibari ambapo awali kuliandaliwa kongamano kubwa lililoandaliwa na Taasisi za Kiislamu kwa kushirikiana na Jumuiya ya Uamsho JUMIKI kwa lengo la kuzungumzia mfumo wa elimu Zanzibar.
Akizungumza na maelfu ya wazanzibari kabla ya kuanza maandamano hayo yaliitwa ni matembezi ya amani, Sheikh Farid alisema wazanzibari wana haki kama walivyokuwa na haki wananchi wengine ulimwenguni kote kudai haki yao ndani ya nchi yao. “Sisi wazanzibari kama wananchi wengine wowote duniani tuna haki ya kikatiba kudai nchi yetu kama walivyodai Sudan ya Kusini, mbona Sudan ya wameweza kujitenda na kupata nchi yao kwa nini sisi kama wazanzibari tusikubaliwe kudai nchi yetu sasa sisi tunampelekea salam katibu mkuu wa umoja wa mataifa kumwambia kuwa wazanzibari sasa wanataka nchi yao” alisisitiza Sheikh Farid huku akiungwa mkono na wananchi hao.
Awali Sheikh Farid alisema salamu hizo anataka zimfikie Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Kin moon ambaye kwamba wazanzibari wamechoshwa na kuwepo ndani ya Muungano ambao umedumu kwa miaka 48 lakini bado ukiwa na kero nyingi na malalamiko ambayo yanaonekana utatuzi wake ni mdogo na usiowezekana ambapo alisema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hauna manufaa yena na wazanzibari.
Katika kuonesha kwamba hawataki tume ya katiba ije kuchukua ya maoni ya katiba mpya Sheikh Farid alisema wanataka kwanza kuamuliwe suala la Muungano kabla ya jambo lolote na kuahidi kwamba wataendelea kufanya makongamano, mihadhara na maandamano kwa kadiri wawezavyo hadi hapo Serikali itakaposikia kilio hicho. “Ujumbe huu tunautoa kwa Ban Kin moon, na kwa ulimwengu mzima lakini pia tunataka rais wetu Dk Shein asikie kilio hiki na Rais Kikwete ambaye yeye ni mtetezi wa haki za binaadamu na pia ni mfuatiliaji wa nchi zinazovunja haki za binaadamu tunataka asikie kilio cha wazanzibari kuwa wanataka nchi yao” alisema.
Alisema juzi wamefanya maombi maalumu ya kumuombea Rais wa Zanzibar lengo likiwa ni kumjaaliwa kheri na awe na maamuzi sahihi juu ya wananchi wa Zanzibar sambamba na kuwaomba Makamu wa Kwanza na makamu wa Pili wa Zanzibar kusikia kilio cha wazanzibari wasiotaka Muungano. “Tunamuomba Rais wetu Dk Shein, Makamu wa Kwanza Maalim Seif na Makamu wa Pili Balozi Seif kwamba sisi wazanzibari tunahitaji Zanzibar huru, tunahitaji heshima ya nchi yetu na tupo tayari kwa lolote kwa hivyo tunataka salamu hizi na ujumbe huu ukufikieni” alisema Sheikh Farid huku akiungwa mkono na maelfu waliohudhuria katika kongamano hilo ambalo awali liliandaliwa kwa lengo la kuzungumzia masuala la elimu na mfumo wake.
Waandamanaji hao walianza kutembea kwa utaratibu maalumu huku magari yakisimama na kuwapisha bila ya kuwepo jeshi la polisi ambapo viongozi wa jumuiya hiyo na wananchi wengine waliongoza utaratibu huo na kutembea katika barabara kwa utaratibu mzuri hadi kumaliza maandamano yao waliyoyaita matembezi ya amani.
Baadae jeshi la polisi lilifika katika eneo ambalo kumefanyika maandamano hayo na kufungua mabango yao ya kuwataka watu kuondoka lakini wakati magari hayo ya polisi matatu yanafika eneo hilo la Kariakoo tayari ummati mkubwa ulikuwa umeshapita katika eneo hilo na hivyo kuingia ndani ya magari yao na kuondoka kwa salama.
Awali akitoa mada katika kongamano hilo, Maalim Abdulhafidh Malelemba alisema sekta ya elimu imekuwa ikidorora Zanzibar kutokana na kukandamizwa na mambo ya Muungano ambapo kila mwaka wanafunzi wanapofanya mitihani hufelishwa kwa makusudi huku idadi ya wanafunzi wanaokwenda katika vyuo vikuu wakiwa kidogo kutokana na kufelishwa katika mitihani ambapo husainiwa na baraza la mithani Tanzania NECTA.
Wakizungumza katika nyakati tofauti katika kongamano hilo, baadhi ya walimu walisema kukosekana kwa baraza la mitihani Zanzibar kusimamia mitihani ya elimu ya juu ndio sababu ya wazanzibari kufelishwa kwa wingi na kushindwa kuingia katika vyuo vikuu kwa kuwa wanafunzi wengi wa Zanzibar hufelishwa.
Walimu hao walitoa ushahidi wa hivi karibuni wa kufelishwa wanafunzi wa kidatu cha nne ambapo walisema lile ni tukio la makusudi lililofanywa na baraza la mitihani ikiwa ni kuwadhoofishwa wanafunzi wa Zanzibar ili wasiendelee katika masomo kwa kuwafelisha.
No comments:
Post a Comment