Mtoto AZRA VUYO JACK akiwa amelala.
AZRA akiwa amepakatwa na baba yake VUYO JACK nje ya mahabusu ya mahakama kuu ya Mbeya.
Baba na Mama AZRA wakiwa na mtoto wao wakisubiri kuingia Mahakamani.
Msamaria mwema EMILY MWAITUKA ndiye aliyejitolea kumhudumia mtoto AZRA huko mahabusu kwa kumpelekea maziwa kila siku.
Hili ndilo gari la wazazi wa AZRA na ambalo lilitumika kubeba madawa hayo.
AZRA VUYO JACK, Mtoto aliyezaliwa mahabusu na kuendelea kukulia mahabusu.
Wakati Tanzania ikiwa imeridhia mkataba wa kimataifa wa kutekeleza na kulinda haki za watoto na kusimamia kwa karibu ulinzi wa haki za binadamu, sasa serikali ina kila sababu ya kuangalia haki za watoto walioko gerezani kwa makosa ya wazazi wao.
Miongoni mwa haki ambazo serikali inapaswa kuchunguza kwa undani na kubainisha kisa kilichosababisha mtoto mdogo wa kike wa miezi sita , Azra Vuyo Jack, ajikute yeye na wazazi wake wakiwa katika mahabusu ya gereza la Ruanda jijini Mbeya wakikabiliwa na tuhuma za kukutwa na dawa za kulevya.
Azra ambaye kwa jina la utani, kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na Mbeya yetu huko gerezani anaitwa Merryciana au bibi jela jina ambalo limezoeleka zaidi mbali ya jina lake halisi alilopewa na wazazi wake la Azra.
Mtoto huyo wa kike aliendelea kukua katika tumbo la mama yake akiwa gerezani, hatimaye alizaliwa salama Julai 15 mwaka jana katika hospitali ya wazazi meta.
Mama yake ni Anastazia Cloete (27) mwenye asili ya kizungu, raia wa Afrika ya kusini.
Cloete alikamatwa mwaka juzi, Novemba katika mpaka wa Tanzania na Zambia , mji mdogo wa Tunduma akiwa mjamzito na kutupwa mahabusu katika gereza hilo hali iliyomfanya aendelee kulea ujauzito wake.
Uchunguzi wa kina uliendelea kufanywa na madaktari wa hospitali hiyo hadi alipojifungua salama.
Uchunguzi wa tukio la mtoto huyo hadi sasa umezusha mwendelezo wa harakati za kihabari na wanaharakati wa haki za binadamu kuona umuhimu wa kuondolewa kwa mtoto huyo ambaye kwa muda wote tangu azaliwe amekuwa akitumia maziwa ya kopo na hanyonyeshwi na mama yake mzazi.
Mmoja wa ya wasamaria wema aliyejitolea kuwahudumia watuhumiwa hao waliyokumbwa na tuhuma za kukutwa na dawa hizo ni Emily Mwaituka ambaye amekuwa akifanya kazi kubwa ili kuhakikisha mtpto anakuwa na afya nzuri kwa kununuliwa makopo mawili ya maziwa kila wiki tangu alipozaliwa julai, mwaka jana.
Mwaituka anasema amekuwa akinunua kopo moja la maziwa ya unga aina ya SMA 1 ambalo huuzwa sh 26000 na anapaswa kununua makopo mawili ili kuweza kumudu mahitaji ya mtoto huyo wa kike ambaye hanyonyi maziwa ya mama yake mzazi anayesubiri hatima ya kesi inayomkabili akiendelea kuwa mahabusu kwenye gereza la Ruanda jijini Mbeya.
Kumbukumbu za tukio hilo tulizonazo zinaonyesha kuwa raia hao wawili wa Afrika ya Kusini, waliokuwa wakiishi mtaa wa 2A Valley Road – Schaapkraal –Capetown walikamatwa na kilo 42 .5 za dawa za kulevya Novemba 18 mwaka juzi katika mpaka wa Tunduma na kufunguliwa – jalada namba TDM/IR/1763/2010.
Katika tukio hilo ambalo Vuyo na Cloete walinaswa na dawa hizo walizozificha kwenye gari aina ya Nissana Hard body yenye namba za usajili CA – 508 – 656 lililokuwa likimilikiwa na Vuyo Jack waliokuwa wakitokea mkoani Morogoro kuelekea Afrika ya Kusini, Cloete alikuwa akisoma katika chuo cha Capetech.
Kwa mujibu wa taarifa za ndani ambazo zimethibitishwa na Mkemia Mkuu wa Serikali dawa hizo za kulevya ni paketi 26 za cocaine zenye uzito wa kilo 28.5 paketi tatu za Heroine zenye uzito wa kilo 3.25 na paketi nane aina ya Morphine zenye uzito wa kilo 3.25, madawa hayo yote yanathamani ya zaidi ya sh bilioni 1.2.