JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WIZARA YA UCHUKUZI
MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA
TAARIFA KWA UMMA NA VYOMBO VYA HABARI
Taarifa hii inatoa mwelekeo wa mabadiliko ya mifumo ya hali ya hewa na mvua kuanzia mwezi Desemba 27, 2011 kuelekea mwaka mpya 2012. Ukanda wa mvua unatarajiwa kuimarika maeneo mengi nchini na mvua zinatarajiwa kuanza kwenye ukanda wa pwani kesho ukiwemo mkoa wa Dar es salaam na kuongezeka kuelekea mwaka mpya 2012.
Mifumo ya hali ya hewa inaonyesha kuimarika kwa hali ya joto la Bahari ya Hindi,sambamba na kuongezeka kwa msukumo wa hewa yenye unyevunyevu kutoka misitu ya Kongo na kusababisha makutano ya upepo katika eneo la mashariki na kusini magharibi mwa nchi kuanzia Disemba 28, 2011 kuelekea mwaka mpya 2012.
Hali hii inatarajiwa kusababisha kuanza kwa vipindi vya mvua kubwa katika maeneo mengi hapa nchini.
Picha tofauti za mawingu na Bahari zilizopigwa kupitia Satelite zikionesha hali ya uwezekano wa kuwepo kwa Mvua kali zinazotarajiwa kunyesha hapa nchini.
Maeneo ya mikoa ya ukanda wa pwani( mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Mtwara, Lindi na Kisiwa cha Unguja,), Nyanda za juu kusini magharibi (Mikoa ya Mbeya, Iringa na Rukwa), kanda ya kati(Mikoa ya Dodoma na Singida) na magharibi mwa nchi (Mikoa ya Kigoma na Tabora) na maeneo machache ya Nyanda za juu kaskazini Mashariki (mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara) yanatarajiwa kuwa na vipindi vya mvua kubwa.
Kufuatia viwango vikubwa vya mvua vilivyonyesha, ongezeko kidogo la mvua linatarajiwa kusababisha mafuriko na uharibifu wa miundombinu. Mamlaka inashauri tahadhari stahiki ziendelee kuzingatiwa.
Maeneo mengine ya nchi yanatarajiwa kupata mvua za kawaida katika kipindi hicho.
Mamlaka ya Hali ya Hewa inaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya Hali ya hewa na athari zake na itaendelea kutoa taarifa na tahadhari kila inapobidi.