Friday, February 10, 2012

* Rais Jakaya Kikwete aendesha kikao cha Baraza la Mawaziri Mkoani Dodoma


Rais JAKAYA KIKWETE akipeana mikono na Mkuu wa Wilaya ya Bahi Bi. BETTY MKWASA mara baada ya kuwasili uwanja wa ndege wa Dodoma.


Rais JAKAYA KIKWETE akiendesha kikao cha Baraza la Mawaziri katika ukumbi wa TAMISEMI mjini Dodoma.

Thursday, February 9, 2012

* Serikali ya Tanzania yamaliza Mgomo wa madaktari

Rais wa Tanzania Dakta JAKAYA KIKWETE akiwa anateta Jambo na Msaidizi wake,Waziri mkuu MIZENGO PINDA

Serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania imewasimamisha kazi Maafisa wa Ngazi za juu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ikiwa ni hatua muhimu ya kumaliza mgomo wa madaktari hapa nchini.

Akitangaza uamuzi wa Serikali Waziri Mkuu MIZENGO PINDA amewataja waliosimamishwa kazi mara moja kuwa ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bi BLANDINA NYONI pamoja na Mganga Mkuu wa Serikali Dakta DEO MTASIWA.

Amesema uamuzi wa kuwasimamisha kazi umefikiwa ili kupisha uchunguzi dhidi yao kwa vile pia wana tuhuma nyingine ambazo ni kinyume na maadili ya kazi na utumishi wa umma.

Waziri Mkuu PINDA amesema wengine wanaotarajiwa kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa kusubiri uamuzi wa Rais, ni pamoja na Waziri wa Afya Dakta HAJI MPONDA na Naibu wake Dakta LUCY NKYA.

Mgomo wa madaktari ambao umedumu kwa takribani wiki tatu sasa umesababisha kuzorota kwa huduma mbalimbali za matibabu katika hospitali za umma na nyingine zikifunga vitengo muhimu.

Madaktari hao wanadai nyongeza ya mishahara, mazingira mazuri ya kazi pamoja na marupurupu mengine ambapo Serikali imekubali kuyashughulikia.

Katika makubaliano na Waziri Mkuu madakatari waliogoma wamekubali kumaliza mgomo ambapo wanatarajiwa kurejea kazini.

Tuesday, February 7, 2012

* Barnaba kwenda Ufaransa kurekodi "Tuachane kwa Wema" pamoja na Fally Ipupa

Barnaba - Msanii wa Muziki wa Bongo fleva

Msanii mahiri katika miondoko ya muziki wa Bongo Flava Barnaba, anatarajia kuondoka nchini Machi 28, mwaka huu kuelekea nchini Ufaransa kwa ajili ya kurekodi kibao chake kipya kiitwacho 'Tuachane kwa Wema, ambacho atamshirikisha mwanamuziki nyota wa muziki wa Dansi Fally Ipupa.

Barnaba, alisema kuwa maandalizi yote ya safari hiyo tayari yamekamilika na tayari amekwishapewa 'Apointment' na moja ya Studio za nchini humo tarehe ya kufika na kurekodi wimbo wake huo.

Aidha Barnaba alisema kuwa wimbo huo utakuwa ni miongoni mwa nyimbo zake zitakazokuwamo katika albam yake mpya itakayokuwa na jumla ya nyimbo 10, ambayo inatarajia kukamilika mwezi wa sita mwaka huu.

''Unajua katika ndoto zangu za kimuziki nimekuwa na ndoto siku nyingi ya kurekodi na mastaa wa ukweli Duniani, na Fally ni mwanzo tu kwani wapo wengine ambao tayari nimeshawasiliana nao pande za mamtoni ambao tayari kama watatu wamekwisha nithitishia kunipa 'shavu' katika miongoni mwa nyimbo zangu kadhaa ambazo nyingine zitakuwa ni katika albam yangu ijayo baada ya hii.

Hata Fally pia alikuwa akitamani kurekodi na mimi tangu nilipo mpagawisha katika moja ya shoo yake alipokuja nchini na kuipenda sauti yangu, kwa hiyo naye nipi ni nafasi yake pekee aliyokuwa akiitamani ambayo amefanikiwa''Barnaba alisema kuwa mbali na wimbo huo lakini pia anatarajia kurekodi video ya wimbo huo, awapo nchini humo iwapo atafanikiwa kumaliza ndani ya muda uliopangwa na mwandaaji wake.

Alizitaja baadhi ya nyimbo zitakazokuwa katika albam hiyo kuwa ni pamoja na Gubegube, Sidhani Kama na Roho si Moyo, ambazo zote tayari zimekwisharekodiwa katika Studio za THT.

* Rais Jakaya Kikwete na Makamu wake Dakta Bilal washuhudia utiaji saini makubaliano wa kudhubiti maharamia



Rais JAKAYA KIKWETE na Makamu wake Dkt MOHAMMED GHARIB BILAL nyuma wakishuhudia zoezi la utiaji saini, wakati Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, HUSSEIN MWINYI akisaini mkataba wa makubaliano (MoU) ya Ushirikiano katika mapambano dhidi ya Maharamia kati ya Tanzania, Afrika Kusini na Msumbiji, wakati wa hafla hiyo iliyofanyika Ikulu Dar es Salaam, Kushoto ni Waziri wa Ulinzi wa Msumbiji, FILIPE JACINTO NYUSI kulia ni Waziri wa Ulinzi wa Afrika ya Kusni, LINDIWE SISULU.

Monday, February 6, 2012

* Rais wa Zanzibar Dakta Ali Shein akutana na Uongozi wa Wizara ya Fedha



Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt ALI MOHAMMED SHEIN akizungumza na Uongozi na watendaji wa Wizara ya nchi, Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, katika Ukumbi wa mikutano Ikulu Mjini Zanzibar.

* Dakta Mohammed Bilal apokea wanachama wapya wa CCM katika maadhimisho ya miaka 35 ya Chama hicho, Kibaha Vijijini


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt MOHAMMED GHARIB BILAL, akipokea kadi ya mwanachama mpya kutoka CUF, OMAR SAID HUNDA, aliyeamua kujiunga na CCM, wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka 35 ya Chama hicho zilizofanyika Wilaya ya Kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani.


Baadhi ya Wanachama wapya waliojiunga na Chama cha Mapinduzi CCM, wakila kiapo baada ya kukabidhiwa kadi zao za uanachama na Makamu wa Rais Dkt MOHAMMED GHARIB BILAL, wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka 35 ya chama hicho.

* Rais Jakaya Kikwete amjulia hali mkuu wa majeshi wa awamu ya Kwanza, Jenerali Ernest Mwita Kyaro


Rais JAKAYA KIKWETE na mkewe mama SALMA KIKWETE wakimjulia hali Mkuu wa Majeshi Mstaafu Jenerali ERNEST MWITA KYARO jijini Mwanza, Jenerali mstaafu KYARO, ambaye alikuwa mkuu wa majeshi katika Serikali ya awamu ya kwanza, amefurahi na kumshukuru sana Rais KIKWETE na mkewe kwa kutembelea.



Rais JAKAYA KIKWETE akiongea na wawakilishi wa kundi moja la wachuuzi machinga wa jijini Mwanza ambao walikwenda Ikulu ndogo ya jiji hilo na kumweleza changamoto zinazowakabili, ikiwa ni pamoja na ukosefu wa mitaji pamoja na taaluma ya kufanyia biashara.

Rais KIKWETE ametoa milioni 10 kwa ajili yawamachinga hao kukopeshana mitaji.