Rais wa Tanzania Dakta JAKAYA KIKWETE akiwa anateta Jambo na Msaidizi wake,Waziri mkuu MIZENGO PINDA |
Serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania imewasimamisha kazi Maafisa wa Ngazi za juu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ikiwa ni hatua muhimu ya kumaliza mgomo wa madaktari hapa nchini.
Akitangaza uamuzi wa Serikali Waziri Mkuu MIZENGO PINDA amewataja waliosimamishwa kazi mara moja kuwa ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bi BLANDINA NYONI pamoja na Mganga Mkuu wa Serikali Dakta DEO MTASIWA.
Amesema uamuzi wa kuwasimamisha kazi umefikiwa ili kupisha uchunguzi dhidi yao kwa vile pia wana tuhuma nyingine ambazo ni kinyume na maadili ya kazi na utumishi wa umma.
Waziri Mkuu PINDA amesema wengine wanaotarajiwa kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa kusubiri uamuzi wa Rais, ni pamoja na Waziri wa Afya Dakta HAJI MPONDA na Naibu wake Dakta LUCY NKYA.
Mgomo wa madaktari ambao umedumu kwa takribani wiki tatu sasa umesababisha kuzorota kwa huduma mbalimbali za matibabu katika hospitali za umma na nyingine zikifunga vitengo muhimu.
Madaktari hao wanadai nyongeza ya mishahara, mazingira mazuri ya kazi pamoja na marupurupu mengine ambapo Serikali imekubali kuyashughulikia.
Katika makubaliano na Waziri Mkuu madakatari waliogoma wamekubali kumaliza mgomo ambapo wanatarajiwa kurejea kazini.
No comments:
Post a Comment