Meneja wa KCB Tanzania tawi la Mwanza ELIAS MWAKATOBE akimkabidhi Afisa Elimu Sekondari Jiji la Mwanza ANNE ALOPA baadhi ya vitabu vyenye thamani ya shilingi Milioni 1.5 vilivyotolewa na benki hiyo kwa shule ya sekondari ya Kangaye wakati wa hafla iliyofanyika Nyamagana jijini Mwanza hivi karibuni.
Mkuu wa kitengo cha Masoko na Mahusiano wa KCB Tanzania Bi CHRISTINE MANYENYE akimkabidhi Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kangaye JOSEPHINE MLUNDWA baadhi ya vitabu vyenye thamani ya shilingi Milioni 1.5 vilivyotolewa na benki hiyo wakati wa hafla iliyofanyika Nyakato jijini Mwanza hivi karibuni, anayeshuhudia katikati ni Mwenyekiti wa Bodi ya shule hiyo JOSEPH NYANDA.
Mkuu wa kitengo cha Masoko na Mahusiano wa KCB Tanzania Bi CHRISTINE MANYENYE akiwakabidhi kaka mkuu wa shule ya sekondari Kangaye MARWA MANG'ANA, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kangaye JOSEPHINE MLUNDWA na dada mkuu GRACE GIMAHENGA baadhi ya vitabu vyenye thamani ya shilingi Milioni 1.5 vilivyotolewa na benki hiyo wakati wa hafla iliyofanyika Nyamagana jijini Mwanza.
Wanafunzi wa kidato cha tatu wa shule ya Sekondari Kangaye iliyopo Nyamagana jijini Mwanza wakifanya mazoezi ya maabara ki-vitendo wakati Benki ya KCB Tanzania ilipokabidhi msaada wa vitabu vya sayansi wenye thamani ya shilingi Milioni 1.5 hivi karibuni.
KCB Tanzania yaomba wanafunzi wawezeshwe ubunifu
Na Mwandishi wetu, Mwanza
Benki ya KCB Tanzania imeiomba serikali kuongeza vifaa vya kufundishia katika shule mbalimbali nchini ili kuwawezesha walimu nchini kuibua vipaji tofauti vya ubunifu walivyonavyo wanafunzi.
Hayo yalisemwa na Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mahusiano wa KCB Tanzania Bi Christine Manyenye hivi karibuni wakati akikabidhi msaada wa vitabu vya masomo ya Sayansi vyenye thamani ya shilingi Milioni 1.5 kwa shule ya Sekondari Kangaye iliyopo Nyamagana jijini Mwanza.
Akifafanua Manyenye alisema kuwa kutokana na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia wanafunzi wengi wameonesha utayari kubuni vitu mbalimbali lakini wanashindwa kuendelea mbele kwa kukosa miongozo ya kufika watakapo.
Vilevile aliongeza kuwa msaada huo wa vitabu vilivyotolewa na KCB Tanzania utawezesha wanafunzi wa Sekondari ya Kangaye kujifunza masuala mbalimbali yatakayowasaidia kubuni bidhaa mbalimbali ambazo sasa zinaagizwa kutoka nje ya nchi.
“Hivi sasa hata kalamu za kuandikia zinaingizwa kutoka nje, hili linasababishwa na wanafunzi kutowezeshwa kuwa wabunifu tangu wakiwa watoto. KCB Tanzania imeliona hili na kuamua kuwekeza katika kusaidia vitabu hivi vya kisayansi ili kukuza uelewa miongoni mwao,” Alisema Manyenye.
Kwa upande wake Afisa Elimu wa Shule za Sekondari Jiji la Mwanza Anne Alopa alisema shule nyingi nchini zinakabiliwa na upungufu wa vifaa vya kiada licha ambapo serikali imekuwa ikijitahidi kulipatia ufumbuzi suala hilo.
Kutokana na hilo Alopa alitumia fursa hiyo kuipongeza Bodi ya Shule ya Sekondari Kangaye kwa kumtafuta mdhamini huyo ambaye tayari ameonesha nia ya kuendelea kuisaidia shule hiyo baada ya awali kujitokeza kupanda miti zaidi ya 3,000 shule hapo.
“Naipongeza KCB Tanzania kwa kuanza kutekeleza ahadi zake za kuisaidia Kangaye, natoa wito kwa uongozi wa shule kuendelea kushirikiana na benki hii ili kuweza kupata misaada zaidi,” alisema Afisa Elimu huyo.
Naye Mkuu wa Shule hiyo Josephine Mlundwa alisema msaada huo wa vitabu kutoka benki hiyo umepunguza mahitaji kwa asilimia 30 na kwamba utawezesha walimu kuongeza kiwango cha ufundishaji kwa wanafunzi.
Mbali na hayo alizitaja changamoto nyingine zinazoikabili shule hiyo kuwa ni umeme, maji, vifaa vya maabara, viti na meza za maabara na za walimu, majengo ya utawala, maktaba, vyoo, nyumba za walimu, maabara kwani sasa wanatumia vyumba vya madarasa kama maabara kwa kufundishia masomo ya Sayansi.