Friday, November 25, 2011

* Kampuni ya Tigo Tanzania yakabidhi Majengo ya madarasa mawili kwa Shule ya Msingi ya Pugu kajiungeni


Mwakilishi wa kampuni ya Tigo ALEX MSIGARA akiongea na wanafunzi wa Shule ya Msingi Pugu Kajiungeni wakati wa kukabidhi madarasa jijini Dar es Salaam, Kulia kwake ni Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Bi. MARIAM KORONGO, kushoto kwake ni Afisa Elimu, Vifaa na Takwimu (W) Ilala ABILAH MCHIA.


Afisa Elimu, ABILAH MCHIA akizungumza na waandishi wa habari na walimu wakati kampuni ya Tigo ilipokuwa ikikabidhi  madarasa mawili ya Shule ya Msingi Pugu Kajiungeni jijini Dar Es Salaam, Kulia kwake ni mwakilishi wa Tigo ALEX MSIGARA na mwalimu mkuu Bi. MARIAM KORONGO.


Mwakilishi wa kampuni ya Tigo, ALEX MSIGARA akimkabidhi mwalimu mkuu wa shule ya msingi Pugu Kajiungeni Bi MARIAM KORONGO madaftari, kalamu za Tigo pamoja na T-shirt.

Tigo yakabidhi madarasa mawili

Tarehe 22 November 2011, Dar es Salaam, Kampuni ya simu za mkononi ya Tigo  imekabidhi madarasa mawili kwa shule ya msingi Pugu Kajiungeni iliyopo eneo la Gongolamboto jijini Dar es salaam baada ya kumaliza ukarabati wa majengo ya shule hiyo yaliyoharibiwa na mlipuko wa mabomu yaliyolipuka katika kambi ya Gongolamboto mwezi May jijini Dar es Salaam.

Akizungumza mara baada ya kukabithi rasmi majengo hayo kwa mwalimu mkuu wa shule hiyo, Afisa viwango na mwakilishi wa kampuni ya simu za mikononi ya Tigo Alex Msigara amesema “Sisi kama kampuni ya simu za mikononi ya Tigo tuliguswa kwa namna ya kipekee na tukio hili hasa ukichukulia kuwa wahanga wakubwa walikuwa ni watoto ambao walitaharuki na kuanza kukimbia huku na huko, na wengine kushindwa kwenda shule kutokana na mjengo kuharibika hali iliyowaondolea amani wakiwa shule”

Alex akaongeza “Nadhani waandishi na wananchi wanaoipenda Tigo watakuwa ni mashahidi kuwa sisi tumekuwa mstari wa mbele katika kuchangia elimu hasa elimu ya msingi ambapo tumeweza kutoa vitabu na vibao vya mapajani siku chache zilizopita kwa baadi ya shule za msingi nchini kwani tunaamini watoto wakikua katika misingi yenye yenye uelekeo mzuri kielimu basi wao ndio watakaoijenga Tanzania nzuri siku za usoni”

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Pugu Kajiungeni Bi Mariam Korongo akitoa shukrani zake kwa Tigo amesema “kwa niaba ya walimu, wazazi wa wanafunzi na wanafunzi wenyewe wa shule ya msingi Pugu Kajiungeni, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa msaada huu wa kutengenezewa madarasa haya mawili. Tunashukuru kuona kwamba taasisi binafsi zinakuwa zinaguswa na matatizo yanayozikumba jamii inayozizunguka kwani hiyo inapunguza mzigo kwa serikali ambayo inafanya juhudi kubwa katika kuhakikisha inaleta maendeleo nchini.”

Mwalimu mkuu akaongeza pia kuwa anafurahi kwamba Tigo wameweza kuwasaidia katika tatizo hilo la ukarabati wa majengo na kuziomba taasisi nyingine kuchangia sekta ya elimu katika shule mbalimbali kwani matatizo yanafanana nchini kote.

Mara baada ya tukio la mlipuko wa mabomu familia za maeneo yale zilipata misukosuko mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupotezana kwa hofu, kuharibika kwa makazi na maeneo ya biashara, Tigo ilitembelea maeneo yale na kujionea jinsi uharibifu ulivyotokea na kuwapa mkono wa pole wahanga na namna ya pekee ikiwa ni pamoja na kuchukua jukumu la kukarabati majengo ya shule yaliyoharibiwa.

No comments:

Post a Comment