Thursday, May 24, 2012

* Dakta Bilal ahudhuria Mkutano wa Wakuu wa nchi Kuhusu maendeleo Barani Afrika



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dakta MOHAMMED GHARIB BILAL akihutubia kwenye mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Maendeleo Endelevu katika Bara la Afrika mjini Gaborone.
 
 
 Na ; Mwandishi Wetu
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Dkt Mohammed Gharib Bilal amemwakilisha Rais Jakaya Kikwete katika mkutano wa Maendeleo Endelevu Afrika unaolenga katika kujumuisha thamani ya Rasilimali Asilia katika kupima maendeleo ya kiuchumi katika nchi za Afrika.
Katika mkutano huo, Tanzania imeunga mkono kuanzishwa kwa mfumo wa kujumuisha thamani ya raslimali asilia ambao utahusishwa kwenye tathmini ya pato la taifa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na  vijavyo.
Makamu wa Rais Akihutubia mkutano huo amesema, mchango wa rasilimali asilia zina nafasi kubwa katika kuchangia katika pato la taifa lakini ili mchango wake utambulike, nchi zinahitajika kuwa na utaratibu wa kuzifanyia tathmini hasa kuhusu matumizi yake na faida zake katika uchumi huku pia athari zake zikitazamwa hasa zile zinazotokana na kupoteza uhalisia wa mazingira ama kuharibu mazingira ya nchi.
Kwa mujibu wa Makamu wa Rais, dhana ya kutathmini mazingira na kujumisha raslimali asilia kwenye hesabu za pato la taifa, kunaweza kusaidia nchi kufikia maamuzi ambayo yataliwezesha taifa kupata maendeleo endelevu hali ambayo itachangia jitihada za kupunguza umaskini na kukuza uchumi.
Dkt. Bilal ameueleza mkutano huo kuwa, Tanzania iliona umuhimu wa raslimali asilia tangu nchi ilipopata uhuru mwaka 1961 ambapo iliweza kutenga asilimia 30 ya eneo la nchi kwa ajili ya wanyama na viumbe hai, Tena ziliwekwa sera nzuri zilizolinda uvunaji wa raslimali hizo kwa manufaa ya taifa.
Makamu wa Rais ameueleza mkutano huo pia kuwa, nchi nyingi za Afrika zinategemea kilimo kama njia kuu ya uchumi na sekta hii bado inategemea mvua huku ikihusisha wakulima wadogo wadogo hali ambayo inaonesha ma mazingira yataharibiwa ni wazi maisha ya wengi yataathirika.
Anasisitiza kuhusu kuwepo kwa mfumo mpya wa kilimo unazingatia kutoharibu rasilimali asilia na wakati huo huo kuhakikisha kuwa mazingira yanabaki kama yalivyo ili yasaidie jamii zijazo.
Katika mkutano huo, Tanzania na Botswana zimepongezwa kwa uhifadhi wa maliasili na mazingira kwa ajili ya kizazi cha sasa na cha baadaye.
Mkutano huo wa pia unahudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka nchi zipatazo 11 wakiwemo Marais Hifikupenye Pohamba wa Namibia, na Bibi Ellen Johnson Sirleaf wa Liberia.
                                                        = = = =

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dakta MOHAMMED GHARIB BILAL akizungumza na Rais wa Liberia Bibi ELLEN JOHNSON SIRLEAF kwenye mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Maendeleo Endelevu Barani Afrika unaofanyika mjini Gaborone.
 
 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dakta MOHAMMED GHARIB BILAL akiwa katika picha ya pamoja na Wakuu wa Nchi pamoja na wawakilishi  kutoka nchi za Afrika waliohudhuria mkutano wa Maendeleo Endelevu katika Bara la Afrika.

No comments:

Post a Comment