Thursday, May 17, 2012

* Mafisango sasa kuagwa TCC Chang'ombe,Badala ya Viwanja vya Leaders


Marehemu PATRICK MAFISANGO


Mwili wa kiungo mahiri wa Simba Sports Club Patrick Mafisango (32), sasa utaagwa kwenye Uwanja wa TCC club, Chang'ombe, Dar es Salaam, kuanzia saa 3:00 asubuhi badala ya Leaders Club, Kinondoni, kama ilivyotangazwa hapo awali.

Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Geoffrey Nyange amesema kwamba wamehamishia shughuli ya kuuga mwili huo Uwanja wa Siga ratiba nyingine zote zinabaki kama ilivyotangazwa awali.

Mafisango amefariki dunia usiku wa kuamkia leo katika eneo la Keko jirani na Chuo cha VETA jijini Dar es Salaam.

Mafisango alifariki kutokana na ajali iliyotokea wakati gari alilokuwa akiendesha lilipogonga mti ulio pembezoni mwa barabara ya Chang’ombe majira ya saa kumi kasorobo alfajiri ambapo Marehemu alifariki papo hapo.

Kwenye gari aliyokuwamo Mafisango, kulikuwapo na abiria wengine wanne lakini ni Mafisango pekee ndiye aliyefariki dunia.

Mwili wa Marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili tayari kwa kusafirishwa kwenda kwao Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC ambako atazikwa.

Ingawa alikuwa na uraia wa Rwanda na akiichezea timu ya taifa ya nchi hiyo Amavubi, Mafisango alikuwa ni mzaliwa na raia wa DRC na uamuzi wa kuzikiwa huko ni wa familia yake.

Msiba wa Mafisango uko katika eneo la Keko Toroli jirani na kituo cha Chang’ombe Maduka Mawili (Njia Panda Sigara).

Mwili wa marehemu unatarajiwa kuagwa kesho Ijumaa saa nne asubuhi katika viwanja vya Leaders, Kinondoni jijini Dar es Salaam kabla ya mwili wake kusafirishwa kwenda Kinshasa majira ya saa kumi jioni.

Mafisango alizaliwa Machi 30, 1980 huko Kinshasa Zaire wakati huo, na ameacha mke na mtoto mmoja wa kiume,anayeitwa Chris Paul, mwenye umri wa miaka mitano.

Mafisango ameichezea Simba kwa msimu mmoja tu akitokea Azam ya Dar es Salaam lakini kabla ya hapo alichezea pia TP Mazembe ya DRC, APR ya Rwanda na pia aliwahi kuwa nahodha wa Amavubi kwa takribani miaka mitano.

Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, Makamu wake, Geofrey Nyange na wajumbe wa kamati ya watendaji wameeleza kusikitishwa kwao na msiba huo mkubwa kwa klabu na wamewataka wana Simba wote kuwa watulivu na kumwombea marehemu Mungu amlaze mahali pema peponi.

Uongozi wa Simba umeahidi kwamba utatoa taarifa nyingine zozote muhimu kwa wananchi ili wafahamu kuhusu msiba huo pale itakapotokea.



No comments:

Post a Comment