Friday, September 16, 2011

Kundi la Muziki wa taarabu la T-Moto limesogeza mbele uzinduzi wa albamu yake ili kuomboleza msiba wa meli ya Mv Spice Islander's




Kundi jipya la Taarab la Tanzania Modern Taarab (T-Moto) limesogeza mbele uzinduzi wake uliokuwa ufanyike Septemba 30 mwaka huu hadi Oktoba 28.

Kundi hilo lililoondoka jijini na kuweka kambi ya maandalizi katika Visiwa vya Zanzibar hivi karibuni limeamua kusimamisha mazoezi yake kwa muda wa wiki moja na nusu kufuatia msiba mkubwa ulioikumba nchi kutokana na ajali ya meli ya Mv SPICE ISLANDER'S iliyozama eneo la Nungwi hivi karibuni na kusababisha vifo vya watu wengi na majeruhi ikiwa ni idadi ambayo haijawahi kutokea ndani ya Visiwa hivyo.

Mkurugenzi wa kundi hilo, AMIN SALMIN ambaye ni mtoto wa Rais Mstaafu wa Zanzibar, SALMIN AMOUR ‘Komandoo’, amesema kutokana na kundi hilo kutambua ukubwa wa msiba huo ulio na idadi kubwa ya vifo vya watu kulinganisha na idadi ndogo ya watu waishio visiwani humo, wameamua kusitisha kambi ya mazoezi yao ikiwa ni sehemu ya kundi hilo kuwa katika maombolezo.

Amesema kuwa wasanii wa kundi hilo wataendelea kubaki kambini bila kuendelea na mazoezi hayo ya maandalizi ya uzinduzi wao, hadi baada ya wiki moja na nusu kuanzia siku ya kwanza kati ya tatu za maombolezo zilizotangazwa na Serikali ya Zanzibar.

Kundi hilo linatarajia kuwasili jijini wiki ijayo kwa ajili ya kuingia studio kurekodi nyimbo zake mbili zilizokwisha kamilika na kurejea tena Zanzibar kuendelea na kambi hiyo

No comments:

Post a Comment